Realtime blog statistics Realtime blog statistics
Scanning..

USINZIBE MDOMO MZEE KINANA MBONA SIKUSOMI?

tiko tiko
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Abdulrahman Kinana.
Tangu alipoteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Novemba 2012, Abdulrahman Kinana amekuwa na staili inayonifurahisha sana. Kwa muda mfupi, amekirejesha chama tawala kule ambako kilistahili kuwa kwa siku zote.
Nilipata fursa ya kukutana naye kwa mahojiano mwanzoni tu mwa uteuzi wake ofisini kwake pale Lumumba. Nilimuuliza maswali mengi kwa kila nilichokuwa na mashaka nacho kuhusu chama chake na nimsifu kwamba niliondoka hapo nikiwa sina chembe ya mashaka.
Anachokifanya leo, aliniambia na kunithibitishia kuwa atakifanya. Kukisogeza chama kwa wahusika, wakulima na wafanyakazi, wanyonge, wanoonewa na wanaonyimwa haki. Leo tunamuona, akifanya ziara katika mikoa mbalimbali, lakini siyo tu akikiimarisha chama, bali pia aliwakumbusha viongozi wa serikali wajibu wao.
Baadhi ya mambo anayoyafanya, sikuwahi kuyaona yakifanywa na makatibu wakuu wengine wote waliofanya kazi na Mwenyekiti Jakaya Mrisho Kikwete. Philip Mangula, Yussuf Makamba na Wilson Mukama, kwangu walikuwa makatibu wakuu wa mazoea, wanachowaza ni tofauti na walichokifanya, walitimiza majukumu yao ofisini, nje ya hapo hawahusiki.
Kinana anawafuata siyo tu wanachama, bali wananchi wote, anawauliza kero zao na kama viongozi wao wanafanya juhudi zozote kuzitatua. Anawaalika wabunge na viongozi wa serikali kushiriki mikutano yake na kuwataka kujibu maswali ya wapiga kura wao. Wengi tumewashuhudia wakiumbuka mbele yake na ilipotokea wakazomewa, haraka walijihami kuwa wanaowazomea ni wapinzani!
Lakini nimeanza kupata mashaka na ziara za Katibu Mkuu Kinana. Kwa mbali, ninaona kama zinamjenga zaidi yeye binafsi kisiasa kuliko matarajio ya wananchi. Hii ni kwa sababu anawajua viongozi mizigo, wanaozurura na wanaoshinda ofisini, lakini yeye kama kiongozi mtendaji wa chama, mbona hawachukulii hatua?
Juzi akiwa Singida, aliwaambia wapiga kura wa Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu kuwa mbunge wao anashindwa kutatua kero zao kwa sababu anazurura ovyo. Kama Katibu Mkuu anafahamu udhaifu huu wa waziri wa serikali inayoundwa na chama chake, nini wajibu wa chama kwa watu kama hawa?
Tatizo letu limeendelea kuwa lilelile, tunajua udhaifu wa watendaji wetu, lakini tunashindwa kuchukua hatua, wepesi wa kusema, waoga wa kuchukua maamuzi, hasa magumu!
tiko tiko

Post a Comment

CodeNirvana
© Haki Zote Zimeifadhiwa Kalamu 1 | designed by tabasamu na ∂αиιєℓι
Code Nirvana
Back To Top